MEYA MATENGO AWAKUTANISHA WADAU WA MAENDELEO KUSHIRIKI IFTAR MAALUM YENYE KULENGA UCHANGIAJI WA MIUNDOMBINU YA MADARASA NA VYOO KWA SHULE ZA MANISPAA YA MOROGORO.
MEYA Manispaa ya Morogoro, Mhe. Khalid Matengo,amewakutanisha wadau wa maendeleo kwa kufuturu iftar Maalum pamoja ikiwa na lengo la kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa miundombinu ya Elimu na Vyoo kwa upande wa Shule za Manispaa ya Morogoro.
Iftar hiyo Maalum imefanyika kwenye Ukumbi wa Biashara Mbaraka Mwinshehe DDC Machi 15 -2026 na kuwakutanisha wadau kwa ajili ya maendeleo ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza katika Iftari hiyo, Mhe. Matengo, amesema Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro limedhamiria kwa dhati kuwaletea Maendeleo wananchi wake hivyo katika kufanikisha hilo nguvu ya wadau inahitajika.
Aidha, Meya Matengo, amemshukuru DC Kilakala kwa kujitoa kwake katika kuhakikisha wadau wanakuwa mstari wa mbele katika kuchangia miradi ya maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, amesema hakuna mtu mwengine wa kuijenga Manispaa ya Morogoro zaidi ya wananchi wenyewe wa Manispaa.
DC Kilakala, amesema Dkt. Samia ameleta fedha nyingi za miradi ya Maendeleo hivyo ni wakati sasa wadau kuendelea kumuunga mkono kuchangia miradi ya maendeleo.
“Sisi watu wa Morogoro tunawajibu wa kuchangia miradi ya maendeleo kwa sababu wanufaika wa kwanza ni sisi na inatugusa moja kwa moja, tumuunge mkono Meya wetu kwa wazo zuri la kuhakikisha Manispaa ya Morogoro inakimbia na kutimiza ndoto yake ya kuwa Jiji” Amesema DC Matengo.
Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Emmanuel Mkongo, amesema Manispaa ya Morogoro itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikiasha miradi yote inakamilika na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu Manispaa ya Morogoro, Edward Mwamotela, amesema ili Manispaa ipige hatua na kufanikisha dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 kuna haja ya kuimarisha huduma ya elimu kwa kuchangia na kuwa na rasilimali watu walioelimika na uwezo wa kufanya kazi kwa tija.
Kwa upande wa wadau hao , ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Jumuiya ya Ahmadiyya Morogoro, Sheikh Abid Mahmood Bhatti,ameahidi kuendelea kudumisha ushirikiano na Manispaa ya Morogoro katika masuala mbalimbali na kushiriki katika ukuzaji wa uchumi kwa manufaa ya Wananchi wa Manispaa ya Morogoro .















Post a Comment