Header Ads

‎ZAIDI YA KM 90 ZA BARABARA KUCHONGWA KUONDOA CHANGAMOTO YA MIUNDOMBINU YA BARABARA MANISPAA YA MOROGORO.

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, amesema Manispaa ya Morogoro inatarajia kuchonga zaidi ya Km 90 za barabara ili kuondoa changamoto ya barabara ambapo imekuwa kilio cha muda mrefu kwa Wananchi.

‎Hayo ameyasema Julai 16-2025 akizindua rasmi zoezi la uchongaji wa barabara Kata ya Lukobe Mtaa wa Tuelewane.

‎Akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika Uzinduzi huo wa uchongaji wa barabara, DC Kilakala, amelishukuru Baraza la Madiwani la Manispaa ya Morogoro Kwa uamuzi wa kuja na muarubaini wa kero za miundombinu ya barabara kwa kununua Greda kupitia mapato ya ndani.

‎DC Kilakala, amesema Manispaa ya Morogoro imekuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara hivyo Greda hilo litakuwa ni muarubaini wa kero za miundombinu ya barabara kwa Kata zote 29 za Manispaa ya Morogoro.

‎Aidha, DC Kilakala, amewataka wataalamu kulitumia Greda hilo kwa malengo yaliyokusudiwa ili Wananchi waendelee kunufaika na matunda ya Kodi zao.

‎" Leo tumezindua Mradi wetu wa kuchonga barabara, nitoe wito kwa wananchi na Viongozi wa Mitaa tutoe Ushirikiano ili kulinda mtambo huu na kuepuka kukwamisha shughuli za mradi unaoendelea kwani  tukikwamisha mradi huu , tutakuwa tumekwamisha Maendeleo ya Wananchi wetu" Amesema DC Kilakala.

‎Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Christopher Komba, amesema greda hili limenunuliwa shillingi bilioni 1.3 kupitia mapato ya ndani, hivyo matarajio yake kuona linakwenda kutatua changamoto ya barabara na kurahisisha mawasiliano ya usafiri kwa Wananchi.

‎Naye Kaimu Meneja wa Tarura Manispaa ya Morogoro, Eng. Boniface Kapumbe, amesema zoezi la uchongaji wa barabara linafanywa na taasisi ya Tarura kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro.

‎Kapumbe , amesema kuwa zoezi hilo litaenda kwa awamu ambapo kila Kata Mtambo huo utapita kwa ajili ya kutatua changamoto ya barabara.

‎Upande wa mwananchi Mtaa wa Tuelewane Kata ya Lukobe, ameishukuru Manispaa ya Morogoro Kwa kutatua kero ya barabara ambapo barabara ya Mtaa huo ilikuwa changamoto na Sasa wanaamini uchongaji wa barabara hiyo itawarahisishia Wananchi huduma ya usafiri kwa urahisi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.