Header Ads

RC MALIMA AIPONGEZA HOSPITALI YA RUFAA YA MOROGORO KWA KUHIMILI WAGONJWA KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA



 

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe.Adam Malima,ameipongeza   Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa kuhimili na  kupokea wagonjwa wengi kwa wakati mmoja kutokana na uwekezaji mkubwa alioufanya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha majengo  na kununua vifaa tiba vya kisasa.

RC Malima  amesema hayo Mei 17, 2025 mara baada ya matembezi ya hisani ya miaka 80 ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo yakiambatana na kaulimbiu isemayo "MIAKA 80 YA UJENZI WA JAMII YENYE AFYA " .

Aidha,RC Malima, amesema uwezo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro umekuwa mkubwa na kuweza kuhimili wagonjwa wengi baada ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa takribani Tsh Bilioni 7.8 kwa ajili ya kuboresha majengo yakiwemo Jengo la mama na Mtoto na vifaa vya kisasa kama vile  CT Scan, Digital X-Ray, Mtambo wa kufua hewa tiba ya oksjeni, Kifaa cha uchunguzi wa sikio, koo na pua, mashine zaidi ya kumi za kuchuja damu (Dialysis).

".. Wagonjwa wote wanapata huduma kwa pamoja na hii ni ishara ya Hospitali hii kuhimili mambo makubwa.." Amesema RC Malima.

Aidha Mhe. Malima ameupongeza uongozi wa Hospitali hiyo kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya jambo linalopelekea kuiheshimisha  hospitali hiyo na kuwatendea haki wana morogoro na watanzania wengine kwa kutoa huduma nzuri na kwa wakati.

Katika hatua nyingine, RC Malima,  amewakumbusha wakazi wa Mkoa huo kushiriki kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili ili waweze kupata haki ya kuchaguliwa na kumchagua kiongozi wanayemtaka na ambaye ni bora katika kuwaongoza na kuwasemea.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu amesema kuanzia Mei 5 hadi 9, 2025 huduma ya afya cheki imefanyika bure, pia upasuaji kwa wale waliogundulika kuhitaji huduma hiyo  ulianza kufanyika kuanzia Mei 12 hadi 16 na kutolewa bure ambapo  jumla ya waliopatiwa huduma hiyo  ni wananchi 3772, wakiwemo 242 waliofanyiwa upasuaji.

Nae Boniventura Mpeka wa kutoka Mvomero kwa niaba ya wananchi wenzake amesema, huduma imayotolewa katika hospitali hiyo ni nzuri na imeboreka kwa ukilinganisha na miaka minne iliyopita, kwa sasa wahudumu wanatoa huduma zao kwa welidi na kutumia vifaa vya kisasa hivyo ameishukuru Serikali kwa kuwaboreshea hospitali hiyo.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.