Header Ads

MAFUNZO YA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA AWAMU YA PILI YATOLEWA MANISPAA YA MOROGORO

\

MANISPAA ya Morogoro imeendesha Mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili  kwa waandishi wasaidizi na waendesha  vifaa vya kibayometriki (BVR) katika ukumbi wa Glonessy Nanenane Kata ya Tungi Mei 14-2025.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo, Afisa Mwandikishaji Jimbo la Morogoro Mjini, Faraja Maduhu ,amewataka wanasemina hao kuzingatia mafunzo hayo na kwenda kufanya kazi kwa ujuzi, uwezo na weledi walionao ili kutekeleza zoezi la Kitaifa la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili.


Maduhu, amewataka Waandikishaji hao wasihodhi zoezi hilo, kwani kama watakutana na changomoto yoyote wafanye mawasiliano na wataalam wa kutoka Kata, Jimbo au Taifa ili kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa kwa ufasaha.

Aidha, amesema uboreshaji huo utahusisha kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa  taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.

Naye Mjumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, Balozi  Omar Ramadhani  Mapuri,  amesema kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume pia ina jukumu la kuandaa Daftari la Awali la Wapiga Kura na kuliweka wazi kwa umma.

Balozi, Mapuri, amesema  lengo la uwekaji wazi wa Daftari hilo ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa.

Mwisho,Balozi Mapuri, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia yale yote wanayofundishwa,kwa kuwa wasikivu na kufuata sheria,kanuni za Uchaguzi.

Aidha amewalekeza wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata kuwasiliana na watumishi wa tume huru ya Uchaguzi endapo watakutana na changamoto yoyote wakati wa utekelezaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la Mpiga kura.

Kauli Mbiu ya Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura 2025 "Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura, ni Msingi wa Uchaguzi Bora ".

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.