KAMATI YA KUDHIBITI UKIMWI MANISPAA YA MOROGORO YATAKA ELIMU ZAIDI KUTOLEWA KWA JAMII PAMOJA NA UANDAAJI BORA WA TAARIFA
KAMATI ya Kudhibiti Virusi vya Ukimwi (VVU) Manispaa ya Morogoro imezitaka Kamati za Kata kwa kushirikiana na wadau kuongeza kasi ya utoaji wa elimu katika makundi mbalimbalipamoja na kuongeza ufanisi wa uandaaji wa taarifa .
Agizo hilo wamelitoa Aprili 30/2024 katika ziara ya Kamati hiyo kwenye Mkutano walioufanya Ukumbi wa Ofisi ya Kata Kichangani.
Akizungumza katika ziara hiyo,Mwenyekiti wa Kamati Diwani wa Kata ya Sabasaba na Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Mohamed Lukwele, amesema mipango yao kwa sasa wanaelekeza nguvu katika kuboresha mipango kazi ngazi ya Kata ili kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI.
"Tumeona zipo changamoto katika Kamati zetu tunakwenda kufanya maboresho pamoja na kuweka mikakati na mipango thabiti ya kuzipa nguvu kamati za Kata ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi, lakini hata uandaaji wa taarifa bado hauridhishi ,tunakwenda kuweka mfumo wa pamoja wa Taarifa kwa Kata zote ili kusiwe na sintofahamu katika uandishi wa taarifa hizo" Amesema Mhe. Lukwele.
Kuhusu rasilimali fedha, Lukwele,amesema wataliingiza katika baraza na kujadili kwa kina ili kuona namna gani ya kufanya uwezeshaji wa Kamati hizo katika kuziongezea nguvu.
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo , wamezitaka Kamati za Kata zifike hadi kwenye vikao vya wazazi shuleni ili ziwaelimishe wazazi kuhusu kuwaweka wazi watoto wao kuhusiana na swala la maambukizi ili wanafunzi hao waweze kujikinga na hata kwa walio nao wajitokeze kwa walimu wao mashuleni ili waweze kupewa huduma na uangalizi.
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Morogoro Mhe. Amina Ziuye, amezitaka Kamati za Kata zinapowasilisha Taarifa zao za Ukimwi basi waambatanishe na taarifa za unyanyasaji wa kijinsia.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Faraja Maduhu, amesema maelekezo yote Kamati ambayo imeyaelekeza watayafanyia kazi.
Naye, Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI Manispaa ya Morogoro, Upendo Elias, amezipongeza Kamati za Kata kwa namna wanavyoratibu zoezi la ufuatiliaji katika maeneo yao ya kazi.
Mwisho, Kamati hiyo imewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya kwani kupima afya kuna faida ya Kujua afya zao na kuweza kupanga mipango yao , kunusuru afya ya mama na mtoto endapo ameathirika na kutoendelea kuambukiza na kupokea maambukizi mapya.
Post a Comment