Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO ITAENDELEA KUTOA MATIBABU BURE KWA WAZEE.


MANISPAA ya Morogoro  itaendelea kusimamia utoaji wa matibabu kwa Wazee bila malipo, upatikanaji wa dawa Hospitalini  na uwepo wa dirisha maalum kwa ajili ya Wazee ili kuwaenzi na kuwaondolea usumbufu.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na  Katibu wa Afya Manispaa ya Morogoro Bertha Mahanga ,akimwakilisha Mganga Mkuu wa  Manispaa ya Morogoro kwa niaba ya Mkurugenzi wakati wa kugawa Vitambulisho katika Makao ya Wazee Fungafunga Kata ya Kichangani.

Aidha, Mahanga , amesema Manispaa ya Morogoro , itaendelea kutoa huduma kwa wazee pasipo kuchangia gharama za matibabu na kuboresha changamoto ambazo zimejitokeza katika utoaji wa huduma hiyo kwa kundi hilo.

 "Sisi sote ni mashahidi wa utolewaji wa huduma za Afya bila malipo kwa Wazee wote,nitoe  wito kwenu kufika kwenye vituo vya huduma za Afya vya Serikali ili kupatiwa huduma bila kuchangia gharama za matibabu"Amesema Mahanga.

Kwa upande wa Afisa Ustawi wa Jamii na Mratibu wa Wazee Manispaa ya Morogoro, Rehema Malimi, amewaomba  Maafisa maendeleo ya jamii wa kila Kata kuwashauri wazazi ambao watoto wao wanaolelewa na wazee kuona umuhimu wa mtoto kuishi na mzazi ili  kuwapunguzia majukumu.

Malimi, amesema kuwa  Wazee wengi wameachiwa watoto na watoto wao au wajukuu. 

Aidha,amesema Malezi ya watoto hao ni jukumu la wazazi wao hivyo ni vema tukawaelimisha watoto na wajukuu zetu juu ya umuhimu wa malezi ya Wazazi kwa watoto. 

 "Kwa kuwa kila Kata kuna  Maafisa  Ustawi wa Jamii niwaombe mfike ili wazazi hawa waweze kuwajibika kama Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 inavyoelekeza".Amesema Malimi.

Mwisho, Malimi, amempongeza Rais Samia kwa kazi nzuri ya kusimamia huduma za afya hususani katika kuwajali Wazee katika suala zima la matibabu bure na kutoa shukrani  kwa viongozi wa Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwaunganisha Wazee katika kuhakikisha wanapatiwa mahitaji yao ya Msingi.

Naye Mwenyekiti wa Wazee Fungafunga, Mzee Joseph Kaniki, ameushukuru Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kutekeleza ugawaji wa Vitambulisho pamoja na hatua wanazoendelea kuzichukua katika kuimarisha Sekta ya afya  hasa kwa wazee.

Hivyo, Mzee Kaniki, amezidi kuchukua nafasi ya  kumuombea Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan  afya njema ili aweze kuiongoza vyema Tanzania katika kufikia maendeleo.

Katika utoaji wa Vitambulisho kwa Wazee wa Fungafunga, jumla ya Wazee 21 wamepigwa picha bure na kukabidhiwa Vitambulisho vyao vya msamaha wa matibabu.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.