JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA MOROGORO MJINI YAADHIMISHA WIKI YA JUMUIYA WAZAZI KWA KUPANDA MITI NA KUFANYA USAFI WA MAZINGIRA
Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Morogoro Mjini imeadhimisha Wiki ya Jumuiya kiwilaya kwa kufanya zoezi la upandaji miti katika Zahanati ya Mji Mpya, Shule ya Msingi Kaloleni pamoja na kufanya usafi wa mazingira Soko la Mji Mpya.
Tukio hilo la maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Kiwilaya limefanyika Kata ya Mji Mpya Mei 08- 2026.
Akizungumza katika tukio hilo, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Morogoro Mjini , Emmanuel Icon Nestory, amewataka wazazi na jamii kwa ujumla kuendelea kuwajibika katika malezi bora ya watoto pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, hususani zile zinazolenga utunzaji wa mazingira.
Aidha, Icon, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza kampeni za upandaji miti, akibainisha kuwa ni njia endelevu ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri jamii kwa sasa.
Hata hivyo, Icon,amesema ipo kila sababu ya kila Mtanzania kujenga utaratibu wa kufanya usafi ili kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusimamia kikamilifu agenda ya mazingira.
Aidha, wajumbe wa jumuiya hiyo pamoja na wanafunzi wameonyesha mshikamano mkubwa kwa kushiriki zoezi hilo, huku wakiahidi kuitunza miti iliyopandwa ili iweze kuwa na manufaa kwa wagonjwa wanaofika katika Zahanati hiyo , jamii inayokizunguka pamoja na kizazi kijacho.
Shughuli hiyo imehusisha viongozi wa jumuiya, wanajumuiya ya Wazazi na jumuiya nyengine,wananchi pamoja na wanafunzi wa shule ya Msingi Kaloleni , ambao walijitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo la kijamii na kimazingira.
Kwa upande wa Mjumbe wa Baraza la Wazazi Mkoa wa Morogoro, Shakeel Mohamed, amesema kila mwananchi anajukumu la kufanya usafi pamoja na kutunza mazingira.
Shakeel,amempongeza Dkt. Samia kwa kuimarisha suala la usafi na kuahidi kuahamasiha wanajumuiya kumuunga mkono katika utendaji wake wa kazi.
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wilaya ya Morogoro Mjini , Sophia Kalinga,amesema Jumuiya itaendelea kusimamia malezi, mazingira na afya katika kuhakikisha mazingira ya binadamu yanapendeza ili kuondokana na uchafu wa mazingira utakaosababisha magonjwa ya malipuko.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mji Mpya, Kombo Mkumilwa,amewataka wana CCM, Wananchi wa Kata ya Mji Mpya kufanya suala la usafi kuwa ni desturi na endelevu huku akiweka msisitizo mkubwa kwa wafanyabiashara wa Soko la Mji Mpya kuafanya usafi katika maeneo yao ya kazi.
Naye Diwani Viti Maalum Manispaa ya Morogoro Mhe. Latifa Ganzel,ameishukuru Jumuiya ya Wazazi kuadhimisha siku hiyo Kata ya Mji mpya huku akiwataka viongozi wa Kata na Mitaa kuendelea na kampeni ya usafi wa kila jumamosi ili kuimarisha usafi wa Kata hiyo.















Post a Comment