Header Ads

MHAGAMA ASISITIZA ULINZI WA VYANZO NA MIUNDOMBINU YA MAJI



MWENYEKITI wa Wauguzi Wastaafu Manispaa ya Morogoro, Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya maji MORUWASA na Diwani Viti Maalum Manispaa ya Morogoro  Mhe. Imakulata Mhagama amewataka wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwa walinzi wa vyanzo vya maji katika maeneo yao ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

Mhe. Mhagama ,ametoa wito huo o wakati akizungumza katika upandaji wa wa miti zaidi ya 2000 pembezoni mwa Bwawa la Mindu Kata ya Kauzeni kupitia umoja wa wauguzi wastaafu na wadau wa mazingira katika kuadhimisha  miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, Mhe. Mhagama, amesema ni jukumu la kila mwananchi  kulinda miundombinu ya maji, kuanzia kwenye vyanzo vya maji hadi kwa watumiaji, bila kusubiri mamlaka za maji kusimamia jukumu hilo peke yao.

Mhe. Mhagama , amesisitiza kuwa miundombinu ya maji, kama vile mabomba, hifadhi za maji lazima vilindwe ili huduma ya maji iwe endelevu kwa wananchi ikiwemo upandaji wa miti.

Naye Meneja wa Mazingira na Uhifadhi wa Mazingira MORUWASA , Eng. Hafidhi Lacha amesema  kuwa suala la kuhakikisha usalama wa maji ni la muhimu ili kumaliza changamoto zinazohusiana na matengenezo ya miundombinu ya mara kwa mara.

Eng. Lacha,amewapongeza Wauguzi wastaafu, TSF, Shirika la Mzinga pamoja na wadau wa mazingira kwa kufanya zoezi hilo la upandaji wa miti kwa lengo la kuhifadhi vyanzo vya maji hususani kwenye Bwawa la Mindu.

Amesema kuwa miti zaidi ya 2000 iliyipandwa katika eneo hilo ni rafiki wa maji huku akisema jukumu kubwa la MORUWASA ni kusimamia upatikanaji wa maji safi na salama kwa uhakika  na usafi wa mazingira .

"Hatuwezi kusambaza maji safi na salama kwa uhakika kama wananchi wataendelea kuharibu vyanzo vya maji, kwahiyo katika kuendeleza, kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji ni wajibu wa wananchi kuvilinda vyanzo hivi" Amesema Eng.  Lacha.

Aidha, Eng.Lacha, ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na shughuli zote zinazokwenda kinyume na uharibifu wa vyanzo vya maji,ikiwemo shughuli za kilimo, kuchoma misitu bila sababu za msingi , mifugo ndani ya mita 60 ya mito na ndani ya mita 500 ya hifadhi ya Bwawa la Mindu

Upande wa Muhifadhi Mwandamizi kutoka TFS Kituo cha Mbegu Morogoro, Herman Ndanzi, amewashukuru wauguzi wastaafu kwa kuwa na fikra kubwa ya kuhifadhi mazingira

Ndanzi, amesema uhifadhi ni shughuli mtambuka hivyo ili agenda ya kuhifadhi mazingira ifanikiwe inahitaji wadau mbalimbali ili kuwa endelevu.

Kwa upande wa Afisa Utumishi Shirika la Mzinga Ronald Mwandambo, amesema Shirika la Mzinga linathamini mazingira hivyo wapo pamoja katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa na kulindwa hususani katika vyanzo vya maji.

Mwandambo, amesisitiza  umuhimu wa kila mwananchi  kuona ana wajibu wa kuwa mlinzi wa maji pamoja na mazingira.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.