OFISI YA RAIS, SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA KWA KUSHIRIKIANA NA CHUO CHA UHASIBU ARUSHA WATOA MAFUNZO YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA KWA WAKURUGENZI UTAWALA NA RASILIMALI WATU WA WIZARA, TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA ,MAKATIBU TAWALA MIKOA NA WILAYA
Mratibu wa Mafunzo ya Maadili ya Uongozi wa Umma kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha , Dkt. Birigitha John, akizungumza katika mafunzo
Katibu Msaidizi ,Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini na Mratibu wa Mafunzo, Gerald Mwaitebele,akizungumza katika mafunzo
OFISI ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma , kwa kushirikiana na Chuo Cha Uhasibu Arusha, wameendesha mafunzo kwa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ,Taasisi na Mashirika ya Umma, Makatibu Tawala wasaidizi wa Mikoa na Wilaya ikiwa ni juhudi za kuhakikisha viongozi hao wanazingatia maadili ya umma na kufuata taratibu na kanuni za utumishi wa umma kama inavyoelekezwa na Serikali.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mhe. Mathew Kirama, Katibu na Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma na kiongozi wa timu ya wawezeshaji wa mafunzo.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Morena , Manispaa ya Morogoro , Aprili 15-2026 na yameendeshwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushirikiana na Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA).
Akizungumza katika mafunzo hayo Mhe. Kirama, amesema kuwa mafunzo hayo pia yatawajenga watumishi wa umma ili waepukane na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka .
Mhe. Kirama , amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea viongozi wa umma ujuzi wa kina kuhusu maadili katika uongozi, utawala bora, matumizi ya fedha za umma, mifumo ya manunuzi, utoaji wa huduma kwa wananchi, na jinsi ya kutambua na kuondoa migogoro ya kimaslahi.
“Kupitia mafunzo haya, tunatarajia kuwa viongozi wetu watakuwa na uelewa mpana wa misingi ya utawala bora na maadili katika utoaji wa huduma kwa umma, uongozi wenye maadili huimarisha imani ya wananchi kwa Serikali na Taasisi zake , wananchi wanapowaona viongozi wao mnatenda haki , uwazi na uadilifu ,huongeza ushirikiano , utiifu wa sharia na mshikamano “ Amesema Mhe. Kirama .
Hata hivyo, Mhe. Kirana , ametoa wito kwa viongozi wa umma kuhakikisha wanafuata wajibu wao pamoja na kuyafanyia kazi mafunzo wanayofundishwa.
Mwisho,amesema wanatarajia kuona matokeo chanya yanayotokana na matunda ya mafunzo hayo.
Kwa upande wa Katibu Msaidizi ,Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini na Mratibu wa Mafunzo, Gerald Mwaitebele, amesema mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kukubwa kuondoa mvutano kati ya madiwani na wataalamu katika Halmashauri mbalimbali.
Aidha, Mwaitebele, amesema mafunzo hayo yemefanyika ikiwa ni awamu ya pili na yote ni matokeo ya ushirikiano kati ya taasisi mbili ikiwemo Ofisi ya Rais , Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha ambazo zimeingia makubaliano ya kushirikiana katika kutoa mafunzo ya Maadili na Utawala bora kwa Viongozi wa Umma, Kutoa ushauri kuhusu masuala yahusuyo Maadili pamoja na kufanya utafiti kuhusu masuala yahusuyo Maadili.
Mwaitebele, amesema kuwa mafunzo hayo pia yatawajenga watumishi wa umma ili waepukane na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kuleta mabadiliko chanya kwenye utendaji wa kila siku katika maeneo yao ya kazi ambayo ni Mamlaka za Serikali za Mitaa .
Amesema kuwa yapo makundi mbalimbali yatakayohusika na mafunzo hayo ikiwemo Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ,Taasisi na Mashirika ya Umma, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Taasisi za Umma na Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma , Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma , Wakuu wa Idara na Vitengo katika Wizara , Idara za Serikali , Taasisi za Umma , Mamlaka za Serikali na Mashirika ya Umma.
“Tukaona ili tuweze kuisaidia serikali tuwakumbushe wanatakiwa kufanya nini tunawasisitiza kufanya kazi kwa pamoja wajue yanaeleweka lengo lao ni nini dira yao ni nini, watumishi wa Umma Wanatakiwa kufanya kazi kwa pamoja ili watende kwa kuwatimizia mahitaji wananchi,wakiwa hawana maeleano itakuwa ngumu ndio maana tukaona tufanye mafunzo haya” Amesema Mwaitebele.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo ya Maadili ya Uongozi wa Umma kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha , Dkt. Birigitha John, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi wa Umma katika utendaji kazi wao.
Naye , Kamishina wa Uhamiaji ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Edward Chogero, amesema kiongozi ni lazima afuate maadili ya utendaji kazi kwani yeye anamilikiwa na umma hivyo ni lazima ahakikishe anavaa vizuri pamoja na matendo yake yanakuwa mazuri.
Katibu Tawala Wilaya ya Kahama, Glory Absalum , ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo, ameipongeza Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushirikiana na Chuo Cha Uhasibu Arusha kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo ni muhimu yenye lengo la kutengeneza ramani ya kujua viongozi wa Umma wanatakiwa waishi vipi na jamii inayowazunguka.









Post a Comment