MAADHIMISHO YA JUMA LA ELIMU YA WATU WAZIMA YAFANA MANISPAA YA MOROGORO
MWENYEKITI wa Kamati ya Elimu, Afya na huduma za Uchumi Manispaa ya Morogoro , Mhe. Majuto Mbuguyu, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa kwa watoto waliopata ujauzito kupata elimu kama wanafunzi wengine lengo likiwa ni kuwasaidia watoto wa kike kuendelea na masomo ili watimize ndoto zao.
Kauli hiyo ameitoa katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Septemba 25-2024 katika viwanja vya stendi ya zamani ya daladala Mjini kati akimwakilisha Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe.Pascal Kihanga.
"Nimpongeze Rais Dkt.Samia kwa kile alichokieleza kwamba watoto wa kike ambao wanakosa Elimu kwa kupata ujauzito wakishajifungua warudi darasani ili waendelee na utaratibu wa kupata Elimu kama wanafunzi wengine" Amesema Mhe Mbuguyu
katika maadhimsiho hayo,Mhe.Mbuguyu,amesema ipo haja sasa kila shule kuwepo na madarasa ya elimu ya watu wazima ili wale walio nje ya mfumo rasmi wa elimu wapate fursa ya kusoma.
Kuhusu kuimarisha ustawi wa elimu ya watu wazima,Mhe. mbuguyu,amesisitiza kuendelea kuongeza majengo ya madarasa ya kimasomo ya ufundi stadi ili kukabiliana na tatizo la ajira pamoja na stadi za kujifunzia yaani kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) pamoja na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuendesha elimu ya watu wazima.
"Maafisa elimu wa Msingi na Sekondari tunawategemea kuanza kuchonoa mada za bajeti katika idara zenu,sisi baraza la madiwani kazi yetu ni kuidhinisha,kaeni pangeni leteni na hakika suala la kutenga bajeti likija kwetu sisi tutalipitisha ili tusiwavunje moyo hawa waalimu ambao wanafundisha watoto wetu" Ameongeza Mhe.Mbuguyu.
Nae Afisa Elimu watu wazima Sekondari Manispaa ya Morogoro, David Malimbwi, amesema maadhimisho hayo yanalenga kutathmini shughuli za elimu ya watu wazima inavyoendeshwa katika Manispaa ya Morogoro kwa kupata taarifa za utekelezaji wa shughuli za elimu ya watu wazima kwa kuonyesha shughuli mbalimbali zinazofanyika katika elimu hiyo.
Malimbwi,amesema kuwa serikali kupitia mpango wa elimu ya sekondari ulitoa fursa kwa wanafunzi wote walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwepo ujauzito na mazingira magumu waweza kujiunga na vituo vya elimu ya watu wazima.
Pia amesisitiza kuwa wananchi wote ambao walikosa kusoma kwenye mfumo rasmi wanatakiwa kujiunga katika vituo ambavyo vipo ndani ya Manispaa ya Morogoro ili waweze kupata uelewa wa kujua kusoma na Kuandika fursa ambayo italeta maendeleo kwa jamii na nchi nzima kwa ujumla.
Maadhimisho ya juma la Elimu ya watu wazima yamefanyika kwa mgeni rasmi kutembelea mabanda mbalimbali kutoka katika vyuo vya VETA, Vikundi mbalimbali na Banda la stadi za kujifunzia.
Maadhimisho hayo kwa mwaka 2024 yamebeba kauli mbiu ya "Ujumuishi katika Elimu bila ukomo kwa Ujuzi, Ustahimilivu, Amani na Maendeleo”
Post a Comment