DIWANI MSUYA AWATAKA WANANCHI KUZINGATIA LISHE BORA
DIWANI wa Kata ya Mbuyuni Manispaa ya Morogoro,Mhe.Samwel Msuya,amewataka wananchi wa Kata hiyo kuzingatia lishe bora kwa makundi yote ya watu kuanzia ngazi ya familia.
Hayo ameyasema akiongea na wananchi wakati wa maadhimisho ya siku ya Lishe ya afya katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024-2025 kwenye eneo la Ofisi ya Kata Septemba 25-2024
Akizungumza na wananchi hao,Mhe. Msuya, amewataka watu wote ndani ya jamii wenye uelewa timamu kufuatilia masuala ya lishe kwa familia nzima.
"... Watoto,kina mama wajawazito, wazee wote ni makundi yanayohitaji kupata lishe kwa kuzingatia makundi matano ya vyakula kwa kipimo sahihi,tusimuachie mama peke yake hata kina baba mna nafasi yenu katika kuhakikisha familia inapata huduma zote za kiafya ikiwemo lishe bora." Amesema Mhe. Msuya.
Mtendaji wa Kata ya Mbuyuni,Sada Mpina,amesema siku ya lishe itakuwa endelevu kwa kila robo ya mwaka kwani ni moja ya vipaumbele vyao vya kutoa elimu ya lishe ili kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto.
Kwa upande wa Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mbuyuni,Alicia Mbaga, amewataka wananchi kuzingatia mlo kamili, watoto kupata chanjo,kina mama wajawazito kuanza kujifuatilia mapema kwa kuhudhuria kliniki punde wanapojigundua ni wajawazito na kunywa maji safi na salama ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuwa na jamii salama yenye afya nzuri.
Naye, Mhudumu kiongozi wa huduma za afya ya Jamii (CHW) Kata ya Mbuyuni, Enock Mkoba, amesema maadhimisho hayo yameongeza chachu ya jamii yao kuhudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma na kupata huduma mbalimbali za afya jambo linalozidi kuimarisha afya zao.
Maadhimisho hayo ya lishe Kata ya Mbuyuni, yamekuwa ya kipekee kwani watoto wamepatiwa uji wa lishe na mtori huku elimu zaidi ya vitendo ikitolewa namna bora ya kupika lishe kamili kwa uwiano sahihi wa makundi yote ya vyakula.
Post a Comment