Header Ads

TAWASANET YAIKABIDHI MANISPAA YA MOROGORO VYOO VYA KISASA VYENYE THAMANI YA MILIONI 43 SHULE YA MSINGI MGULU WA NDEGE



TAASISI  isiyo ya Kiserikali ya TAWASANET ,imeikabidhi Manispaa ya Morogoro  vyoo viwili vya kisasa ikiwemo choo cha wavulana na wasichana shule ya Msingi Mgulu wa Ndege Kata ya Mkundi.

Tukio hilo la makabidhiano ya vyoo  limefanyika Julai 17-2024 ambapo katika makabidhiano kilipokelewa na mwakilishi wa Mkurugenzi ambaye ni Mchumi wa Manispaa ya Morogoro , Edward Mwamotela akiongozana na Afisa Elimu Msingi, Gregory Fabian.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi choo hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWASANET , Mhandisi Herbet Kashililah, amesema lengo la TAWASANET ni kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa maji safi na salama shuleni ikiwemo pamoja na kuboresha miundombinu ya vyoo  ikiwemo ujenzi wa vyoo vya kisasa ambavyo wameendelea kuvijenga katika maeneo mbalimbali nchini.

Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Edward Mwamotela, amewataka waalimu kwa kushirikiana na wanafunzi kulinda  vyoo hivyo vyenye miundombinu ya kisasa ili kiweze kudumu kwa muda mrefu, sambamba na kuzingatia usafi katika matumizi.

Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro, Gregory Fabian,  ameowaomba Wazazi kuwahimiza watoto kwenda shule mara baada ya kupata hedhi kwani mabadiliko hayo yanazuilika wakiwa shuleni kutokana  na kuwa na chumba maalum ambacho kitatumika kwa wanafunzi hao wanapoingia kwenye hedhi.

Naye Mratibu wa TAWASANET Taifa,Emmanuel Jackson, amesema vyoo hivyo vimegharimu kiasi cha milioni 43 ambapo miundombinu ya watumiaji wote ikiwemo watu wenye mahitaji maalum imezingatiwa.

Pia, Emmanuel,amesema kwa upande wa vyoo vya wanawake wameweka choo maalum ambacho kitatumika kwa wasichana ambao  wameingia hedhi kutokana na mabadiliko ya kimwili.

Aidha, Emmanuel,amesema  kuwa tafiti zinaonesha kuwa mtoto wa kike anakosa masomo siku 4 hadi 5 kila mwezi kutokana na ukosefu wa huduma ya vyoo bora na maji salama na safi shuleni ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Miongoni mwa malengo hayo ni lile lengo namba 4: linalohamasisha kuhusu Elimu Bora, Lengo la 5: linalo hamasisha juu ya Usawa wa Kijinsi na lengo namba 6: kuhusu Maji Safi na Salama.

“Huu ni mwanzo tu bado tuna malengo ya kusaidia na shule nyingine , tunataka vyoo hivi viwe vya mfano hususani upande wa mtoto wa kike, TAWASANET tumeguswa  na jitihada hizi, tumeona nasisi tuunge mkono jitihada za Manispaa yetu kwa kuwajengea Choo hiki cha Kisasa ili kuhakikisha mtoto wa kike anawekewa mazingira rafiki anapokuwa shuleni ili aweze kuhudhuria siku za masomo kwa ukamilifu kama ilivyokuwa kwa mtoto wa kiume kwani “Ukimkomboa mtoto wa kike umekomboa Taifa zima” Ameongeza Emmanuel.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.