Header Ads

DC KILAKALA AWATAKA WASHIRIKI MAFUNZO UFUGAJI KUKU WA NYAMA BILA DAWA KUSAMBAZA TEKNOLOJIA HIYO KWA WANANCHI KUPUNGUZA USUGU WA VIMELEA VYA MAGONJWA KWA BINADAMU.





MKUU wa Wilaya ya Morogoro,Mhe. Mussa Kilakala,amewataka wafugaji wa kuku bila kutumia dawa kusambaza teknolojia hiyo kwa wananchi wa Wilaya ya Morogoro ili kuepusha Usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya Dawa ,UVIDA au (AMR).

Hayo,ameyasema katika Mahafali ya kwanza ya wafugaji washiriki wa shamba  darasa la ufugaji bora wa kuku  wa nyama bila bila Dawa katika eneo la Polister Klabu Machi 21-2025 ambapo kuku hao wanakuwa ndani ya wiki 5 sawa na siku 35

“Tunataka mradi huu usambae Wilaya nzima, tutakaa Pamoja na wafugaji , Kila mmoja atakuwa na wanafunzi wake atakaowanufaisha maarifa ambayo FAO imempatia, hivyo mradi utawafikia watu wengi zaidi ya wanufaika wa moja kwa moja.”Amesema DC KIlakala.

Aidha,DC Kilakala,ameishukuru Serikali chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwa kuwekeza nguvu katika mradi huo na kuwafanya wafugaji kujifunza ufugaji wa kuku hao bila malipo.

Meya Manispaa ya Morogoro,Mhe.Pascal Kihanga, amewataka wafugaji hao kukaa kikao cha pamoja  kusaidia teknolojia hiyo ya ufugaji ienee kwa Kata zote za Manispaa ya Morogoro.

Mhe. Kihanga, amesema FAO ,wamewarahisishia kupata vikundi vya mikopo vyenye sifa ya kukopesheka kutokana na walivyojiandaa.

“Tunawashukuru FAO, wameturahisishia vikundi vyetu kukopesheka kwa urahisi,hawa watu katika mikopo tunawapa vipaumbele kwa kuwa wameonesha kuna kitu wanafanya “ Amesema Kihanga.

Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maeneo ya ufugaji,Mhe. Kihanga ,amesema kuwa Manispaa ina maeneo makubwa hivyo vikundi vijipange watapatiwa maeneo rafiki kwa ajili ya ufugaji.

Kwa upande wa Mratibu wa Mradi wa ufugaji kuku bila kutumia dawa kutoka FAO nchini Tanzania, Dkt.Elibariki Mwakapeje,amesema ufugaji huo unahusisha kinga zaidi kuepusha kuku kuambukizwa magonjwa kwa kuzingatia usafi na kutumia vifaa kinga, lengo ni kuepusha Usugu wa , Vimelea vya magonjwa dhidi ya Dawa, UVIDA au  (AMR) kwa lugha ya kiingereza.


Dkt.Elibariki,amesema Mradi unatekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvivu kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki ambapo utekelezaji wake unafanyika  mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Arusha.

Naye ,Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Manispaa ya Morogoro, Dkt. Tito Kagize,amesema Idara yao wataendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa wafugaji hao ili waweze kutimiza malengo yao.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.