VIONGOZI KATA YA MWEMBESONGO WAHAMASISHA USAFI WA MAZINGIRA,WANANCHI KUJIKINGA NA CORONA.
VIONGOZI wa ngazi mbalimbali katika Kata ya Mwembesongo Manispaa ya Morogor0, wameshiriki kuhamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira pamoja na kuwahimiza kuchukua tahadhari ili kukabiliana na janga la Corona.
Tukio hilo la ufanyaji usafi limefanyika leo Agosti 28/2021 katika eneo la Mfereji wa Anti Malaria.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria katika siku hiyo ya usafi wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwembesongo, Amina Said, amesema viongozi hao wameamua kuhamasisha usafi na wananchi kuendelea kutoa elimu juu ya kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Corona kwa kuvaa barakoa na kunawa maji kwa sabuni na maji tiririka.
"Leo tumeamua kuhamasishana na Wananchi wetu kwa ajili ya kufanya usafi , hata Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan ,ametuhamasisha tufanye usafi lakini licha ya kufanya usafi bado kuna haja ya kuweza kuchukua tahahadhari kwa ajili ya Corona, hivyo tumekuja kuwaambia wananchi umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya na watalaamu wa afya lakini kufanya usafi katika maeneo yao yanayowazunguka" Amesema Amina Said.
"Pia tumekuja kuhamasisha usafi, kwa hiyo leo viongozi wa Kata ya Mwembesongo, pamoja na wananchi tumekutana kufanya safi wa pamoja katika eneo hili la mfereji wa Anti Malaria, hali ya usafi Kata ya Mwembesongo sio mbaya lakini ni vema tukaendelea kusimamia kwani tusipoasimamia uchafu utakuwa mwingi na kuhatarisha afya za wananchi" Ameongeza Amina Said.
Katika hatua nyengine, amesema wangetarajia kuwa na Diwani na Diwani Viti Maalum wa Kata hiyo lakini kutokana na Diwani wa Kata hiyo kuwa na matatizo ya kiafya wameshindwa kujumuika nao.
Aidha wakati wakiendelea kuhamasisha usafi, alichukua fursa ya kuwakaribisha Wananchi katika kujumuika kusheherekea Siku ya Lishe na Afya iliyofanyika leo Agosti 28/2021 katika Ofisi ya Kata .
Miongoni mwa viongozi walioshiriki kufanya usafi kwa kushirikiana na wananchi wa Kata ya Mwembesongo, ni pamoja na Maafisa Watendaji wa Mitaa, Maafisa Afya, Afisa Elimu , Mifugo pamoja na Maendeleo ya Jamii na waalikwa kutoka Kata nyengine.
Post a Comment