Header Ads

DC MSANDO AIPONGEZA KATA YA KILAKALA KUWA YA KWANZA KUTEKELEZA AGIZO LA KAMPENI YA TOKOMEZA ZERO WILAYA YA MOROGORO..

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, akizungumza katika Kikao maalum cha kujadili Kambi maalum ya wanafunzi wa kidato cha nne Kata ya Kilakala  kwa ajili ya mitihani ya Taifa.(wapili kushoto) Diwani wa Kata ya Kilakala, Mhe. Marco Kanga (kushoto) Diwani Viti Maalum Mwanaidi Ngurungu (kulia) Mtendaji wa Kata ya Kilakala , Bright Sospeter.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando,akisaini kitabu cha wageni.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, ameipongeza Kata ya Kilakala kwa kuwa Kata ya kwanza katika kutekeleza agizo la kampeni ya kutokomeza sifuri na kuongeza ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne katika Wilaya ya Morogoro.

Pongezi  hiyo ameitoa Agosti 05/2021 wakati wa kikao maalum cha kujadili Kambi Maalum ya wanafunzi 120 kutoka shule mbili za Sekondari Kata ya Kilakala ikiwamo shule ya Kingalu pamoja na Lupanga kwenye Ukumbi mdogo wa mikutano Chuo cha Ualimu Kigurunyembe.

Akizungumza na Viongozi na baadhi ya Waalimu waliojitokeza katika Mkutano huo wa kuandaa kambi maalum ya kujiandaa na mitihani ya Kidato cha Nne, DC Msando, amesema kuwa lengo la Kampeni hiyo ni kwa aijili ya kuongeza ufaulu na kuondoa kabisa zero Wilaya ya Morogoro.

“Kambi hii  ni muhimu sana hususani katika kipindi hiki cha mitihani ya Taifa ya Kidato cha nne, tunajua Wako wanafunzi wengine ambao hutembea umbali wa kilomita ndefu kufika shuleni, hivyo tunaamini uwepo wa kambi na kuwaweka pamoja wanafunzi katika kipindi hiki kutasaidia kuweza kujiandaa vizuri na mitihani yao,” Amesema DC Msando.

"Ukimsaidia mtoto akaweza kupata elimu unakuwa umeweza kusaidia Tanzania nzima,na mimi kuanzia sasa nataka tuanze  na kidato cha nne  tufute hizo zero na zisiwepo kabisa, Katika kuhakikisha hii linatimia kuna mambo mengi ambayo tutafanya kwa kushirikiana na wadau wote wa elimu nchini ." Ameongeza DC Msando.

DC Msando, amesema Kampeni hiyo itafanyika katika Kata zote zilizopo Wilaya ya Morogoro.

Naye Diwani wa Kata ya Kilakala , Mhe. Marco Kanga, amesema mbali ya kuwa na kambi hiyo pia wanatarajia kuboresha miundombinu katika shule zote za sekondari ikiwamo eneo ambalo litatumika Kambi Maalum.

Mhe. Kanga, amesema kuwa Kambi Maalum ya tokomeza zero na ongezeko la ufaulu linatarajia kuanza hivi karibuni ikiwa ni kambi ya miezi 2 kuanzia Septemba hadi Oktoba  ya maandalizi ya Mitihani ya Taifa ya kidato cha Nne.

Mpaka sasa maandalizi ya Kambi hayo yanaendelea ambapo DC Msando, amewataka Wenyeviti wa Mitaa, Wazazi pamoja na Wadau wa maendeleo kushikana kwa pamoja katika kuwezesha kambi hiyo.

Bajeti ya Kambi inatagemea kuwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya Agosti 9/2021 ili kuona namna ya kuiboresha na kuongeza ufanisi wa Kambi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.