BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA MOROGORO LAADHIMIA KUUNDA KAMATI YA UFUATILIAJI WA DENI LA STENDI YA MSAMVU
BARAZA LA MADIWANI
MANISPAA YA MOROGORO LAADHIMIA KUUNDA KAMATI YA UFUATILIAJI WA DENI LA STENDI
YA MSAMVU
BARAZA la Madiwani Manispaa
ya Morogoro limeadhimia kuunda kamati maalum ambayo itakuwa na jukumu la kwenda
Ofisi ya Rais Tamisemi kukutana na Waziri wa Tamisemi Mh. Mohamed Mchengerwa
ili kuona namna ya kujadili deni la shilingi Bilioni 20 linaloikabili Manispaa
hiyo kutokana na ujenzi wa Stendi ya Mabasi Msamvu.
Hayo yamejiri Aprili
30-2025 katika Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani lililofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro.
“Mkurugenzi amepokea
barua kutoka Ofisi ya Tamisemi ikimtaka Manispaa kulipa deni la Bilioni
20 la ujenzi wa Stendi ya Msamvu , baada ya kupokea barua la Baraza la
Madiwani tumeadhimia kuunda kamati ili tukutane na viongozi wetu
watusaidie kupata kibali cha kukutana naWaziri wa Tamisemi, ili kuketi
pamoja kuona namna ya deni hilo linalipwaje, Rais wetu ni msikivu sana,
tunaimani kubwa katika mazungumzo yetu hili deni atatusaidia kwani deni hilo
sio la viongozi bali ni deni la wananchi wote wa Manispaa ya Morogoro ambapo
tutalazimika kuacha maendeleo mengine kulipa deni hili kupitia fedha za mapato
ya ndani” Amesema Meya Kihanga.
Naye Diwani wa Kata ya
Kihonda, Mhe. Hamisi Kilongo,amesema wananchi wa Manispaa ya Morogoro wana
tunaomba Rais Dkt. Samia aone namna ya kutusaidia kwani Morogoro imekuwa
kinara wa kuongoza kwa kura za Rais , hivyo deni ambalo lipo mbele ni kubwa na
linaweza kutukwamisha shughuli nyingi za maendeleo.
“ Tunaimani na Rais
wetu,amefanya makubwa sana kwenye Mkoa wetu wa Morogoro hususani Manispaa ya
Morogoro,tumepokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo,kwa hili la deni la
Bilioni 20,tunamuomba sana Mhe. Rais alisimamie vyema, kwani bado mapato yetu
ni madogo,tukilipa deni itafanya maendeleo ya Manispaa kusimama”Amesema Mhe. Kilongo.
Kwa upande wa Diwani wa
Kata ya Mafiga Mhe. Thomas Butabile, amesema Dkt Samia amejenga Stendi bora za
kisasa, na amekuwa mstari wa mbele katika kuwaletea maendeleo wananchi,hivyo
ameomba kuwafikiria zaidi Manispaa juu ya deni hilo ambalo ni mzigo mkubwa
kwani bajeti ya Manispaa haijitoshelezi na hata zile ndoto za kuwa Jiji
zitakuwa zimegonga mwamba.
Ikumbukwe kwamba Ujenzi
wa Stendi ya Msmavu, umekuja kufuatia Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana
na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa
(LAPF) kuunda Kampuni ya ubia iliyojulikana kama Msamvu
Properties Company (T) Limited ambayo ilikuwa na jukumu la kusimamia shughuli
zote za stendi ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa ushuru wa stendi, ujenzi na
uendeshaji wa miradi yote itakayokuwa inatekelezwa na Kampuni kwa niaba ya
taasisi hizo mbili.
Post a Comment