Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA HUKU WADAU, JAMII NA WAZAZI WAKIASWA KULINDA MAADILI NA ULINZI WA MTOTO


KATIKA Kuadhimisha siku ya kimataifa ya mtoto wa Afrika inayoadhimishwa Juni 16 kila mwaka, Wazazi na jamii kwa ujumla wametakiwa kushirikiana katika ulinzi wa mtoto kwa kuhakikisha wanatenga muda wa kuzungumza na watoto na kufahamu changamoto wanazopitia ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili na kuwasaidia kufikia malengo yao kwa maendeleo ya baadaye.

Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga akiwa mgeni rasmi  katika Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika  Ukumbi wa Manispaa ya Morogoro Ofisi Kuu Juni 16/2024.

Mhe. Kihanga, amewaomba wazazi na jamii kutenga muda wa kuzungumza na watoto ili kujua changamoto zinazowakabili na hiyo na pamoja wazazi kuepuka migogoro ya kifamilia ili kumlinda mtoto dhidi msongo wa mawazo inayotokana na migogoro anayoishuhudia ndani ya familia hali inayopelekea baadhi ya watoto kujidhuru au kubadilika kitabia.
 
“Manispaa imeandaa maadhimisho haya kwa kushirikiana na wadau  ikiwa ni sehemu ya njia ya kupaza sauti na kuonesha utetezi wetu kwa watoto, Tunafanya kazi na watoto wanaoishi kwenye mazingira ya umasikini uliokithiri na mwaka huu tumejikita katika elimu jumuishi kwa mtoto ambayo lazima izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi na kwa upande wa wazazi na jamii wanatakiwa kushirikiana bega kwa bega na watoto kwa kuhakikisha mustakabali wao unakuwa mzuri.” Amesema Kihanga.

Mwisho, Kihanga,  ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kushirikiana na Asasi mbalimbali katika kuhakikisha mtoto wa Afrika anakombolewa katika utumwa wa kifikra na uchumi na nyanja mbalimbali ili kuweza kujenga jamii iliyo bora.

Akifafanua kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘Elimu Jumuishi kwa Watoto Kuzingatie Ujuzi, Maadili na Stadi za Kazi ,Mhe. Kihanga  amewataka wazazi na  Jamii Katika Kumsaidia Mtoto katika Kufikia Malengo yake kwa Maendeleo ya Baadaye.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Christopher Komba, amesema, maadhimisho hayo yataangazia jukumu la wazazi na walezi pamoja na jamii kwa ujumla katika maendeleo ya mtoto kupitia elimu.

“ Majadiliano yataangazia masuala ya ujuzi, maadili pamoja na stadi za kazi na hii ni pamoja na kuhimiza jamii kuwaongoza watoto katika kutafikia mafanikio yao hapo baadaye.” Amesema Komba.

Komba, amewashukuru wadau wote , wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha wa kuhakikisha maadhimisho ya Mtoto wa Afrika Duniani yanafanyika kikamilifu.

Aidha amesema wanazingatia muongozo wa Taifa unatoa mweleko wa namna ya kuwafundisha watoto dhidi ya mmomonyoko wa maadili na kumfanya mtoto aweze kusimama katika haki zake.

Naye Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa kitengo cha Maendeleo ya Jamii anayehusika na Dawati la mtoto  Manispaa ya Morogoro , Joyce Mugambi,  amesema, wamejikita katika nyenzo ya elimu kwa kuwa humpatia mtoto mwanga, ujuzi na maarifa ya kuweza kutambua alipo na namna ya kupambana dhidi ya hali iliyopo kwa ubora wa baadaye.

Mugambi amesema katika kumwendeleza mtoto dawati hilo humsaidia mtoto katika shughuli za shule na jamii kwa ustawi wao kwa kuhakikisha analindwa katika kufikia ndoto zao.

Aidha, Mugambi amesema, kupitia mabaraza ya watoto, majukwaa na klabu za watoto wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali kuhusiana ma malezi, utu wema, uongozi na maadili ili kuwalinda dhidi ya mabadiliko ya teknolojia katika makuzi yao.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.